NA JACKSON, MWANDU MUYI
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza kuwa kuokoka ni nini hasa na ni kweli kunawezekana hapa duniani. Swali hili limewafanya wengine kutomwamini Bwana Yesu kuwa ni mwokozi wa maisha yao maana hawajui kuwa kuokoka ni hapa duniani, lakini ukweli ndio huo kwamba wokovu tunaupata hapa duniani.
"Kuokoka" ni kumwamini Bwana Yesu kwa moyo wako na kukiri kwa kinywa chako kuwa alikuja katika mwili na anao uwezo wa kukusamehe dhambi zako zote ulizotenda haijalishi ni kubwa kivipi, (Rum 10:9)na anaweza kukuokoa na taabu mbalimbali za hapa duniani, (Mt 11:28) na kukufikisha Mbinguni salama, maana alikuja ili tuwe na uzima wa milele (Yoh 3:16).
Mk 16:16 inaeleza kuwa, "aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa". Hivyo hapa tunagundua kuwa ukimwamini Bwawna Yesu utakuwa umeokoka, hutahukumiwa tofauti na hapo utahukumiwa!
Mt 1:21 inaeleza utabiri wa kuzaliwa kwa Bwana Yesu, na kazi atakayoifanya hapa duniani, ("Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao") kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya (Isa 7:14).
Mdo 2:21 inaeleza kuwa, "Na kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa" ikimaanisha kwamba atakayemwita Bwana Yesu katika shida zake, na dhambi zake ataokolewa (ataokoka). mtu anaweza kumwita Bwana Yesu akiwa duniani kabla hajafa, akifa nafasi hiyo haipo tena! hivyo kuokoka ni hapa duniani.
Nyakati za Mitume wa Bwana Yesu, baada ya Yesu kupaa mbinguni, watu wengi walikuwa wakiokoka au wakiokolewa maana walimwamini Bwana Yesu kutokana na mahubiri na Mafundisho waliyopatiwa na mitume (Mdo 2:46-47), lakini si nyakati hizo tuu, hadi sasa Bwana Yesu anatenda kazi hiyo ya kuokoa watu waliopotea (wenye dhambi, walio upande wa adui shetani) na wenye shida.
Zab 16:3, "Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao". Hapa watu wanaotajwa ni watu waliookoka, waliopo hapa duniani, wanaoishi maisha ya kumpendeza Mungu na kujiepusha na uovu, hawa ndio Mungu aliopendezwa nao, hivyo kuokoka ni hapa duniani.
Mt 28:19-20 inatoa agizo kwa watu ambao tayari wameokoka kuwa wawafundishe na wengine waliopo ulimwenguni au duniani kuwa yawapasa nao wamwamini Bwana Yesu (waokoke), wabatizwe kwa maji mengi kwa Jina la Baba na la Mwana (Yesu) na Roho Mtakatifu na pia wayashike yote ambayo Bwana Yeseu aliwafundisha Mitume, au yote ambayo tuliookoka tumefundishwa na Watumishi wa Mungu wachungaji wetu ili kwamba nao wawe sawa nasi, tuwe wanafunzi wa Yesu sote, na huko ndiko kuokoka, kumwamini Bwana Yesu katika Yote na kufuata maagizo yake.
Baada ya kuzaliwa tu Bwana Yeesu katika mji wa Bethlehemu, malaika wa BWANA waliwajia watu waliokuwa wakichunga mifugo yao na kuwaamnia kuwa, "maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa; kwa ajili yetu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana". (Lk 2:9-11). Neno "Mwokozi" lina maana ya "anayeweza kuokoa", au "anayewaokoa watu", au "anayefanya watu waokoke"; hivyo ukimwamini Bwana Yeesu kwa moyo wako na Kukiri kwa kinywa chako kuwa ni mwokozi wa maisha yako utaokoka, hapahapa duniani.
Basi baada ya kuokoka,mtu huanza kuishi maisha mapya katika ufalme mwingine mpya wa nuru (2Kor 5:17, Kol 1:13).
Najua sasa umefahamu kwa sehemu kuwa kuokoka ni hapa duniani, hivyo chukua uamzi sasa wa kufanya hivyo; kwa wewe mwenzangu ambaye tayari umeshaokoka au umeshampa Bwana Yesu maisha yako, basi tujitahidi kumtunza yeye maisha yetu yote, maana hatujakamilika bado, yeye ndiye mkamilishaji mkuu, na utimilifu wa wokovu wetu sasa ni pale tutakapohesabiwa haki na kupewa uzima wa milele, na kuishi naye Mwokozi wetu Mbinguni milele na milele (Mt 24:13, Ufu21:1-7).
MUNGU AKUBARIKI SANA USOMAYE UJUMBE HUU.
No comments:
Post a Comment